Last Updated on 10/03/2022 by Tabibu Fadhili Paulo
Vyakula vya asubuhi vya mgonjwa wa vidonda vya tumbo
Mgonjwa wa vidonda vya tumbo ni lazima uwe makini sana na chakula unachokula kila siku.
Chakula unachokula kila siku kitaamua ikiwa dawa unayotumia kutibu vidonda vya tumbo itakuponya na kukuacha huna vidonda tena milele au ndiyo utapata nafuu ya muda mfupi tu na baadaye utaendelea kuumwa vidonda tena na tena mpaka utakapokata tamaa na kutoamini kama kuna kupona vidonda vya tumbo.
Chakula unachokula kinapaswa kiwe ni dawa pia.
Ulivyo ni kile unachokula kila siku.
Usile tu ili kushiba au kwa sababu unasikia njaa.
Lazima ujuwe hiki unachokula ni nini, kina kazi gani mwilini na je kinaweza kusaidia kupona au kupunguza makali ya vidonda vya tumbo?
Hiki unachokula ni nini?
Kina kazi gani mwilini?
Je kinaweza kusaidia japo kupunguza gesi au kupunguza asidi tumboni na kutibu vidonda au majeraha tumboni?.
Kanuni ya jumla ya chakula cha mgonjwa wa vidonda vya tumbo kwa siku ni kuwa asilimia 80 ya chakula unachokula katika siku iwe ni mboga za majani na matunda.
Hii ni kusema kama jumla ya chakula unachokula kwa siku kina ujazo wa kilo 3 basi kilo 2 na nusu ziwe ni matunda na mboga za majani na nusu kilo iliyobaki ndiyo viwe vyakula vingine.
Cha kwanza kabisa unapoamka kitandani asubuhi, yaani ile unatua tu mguu kutoka kitandani ni maji ya kunywa.
Ukiamka tu kabla hata ya mswaki unapaswa unywe maji glasi moja (robo lita) au glasi 2 (nusu lita) ndiyo uendelee na maandalizi ya chai na kupiga mswaki na shughuli zingine.
Na hii ni kwa wote haijalishi unaishi sehemu zenye baridi au joto ni lazima kunywa maji.
Maji ya kawaida siyo ya kwenye friji wala siyo ya moto au ya uvuguvugu.
Maji ya kawaida (room temperature).
Pia nimeona wengine wanapenda kuchemsha maji yao ya kunywa ili kuondoa vijidudu.
Mimi binafsi nashauri maji mazuri ya kunywa ni yale ya kuchujwa na siyo ya kuchemshwa.
Kama una hela unaweza kununua filta maalumu za kuchujia maji na kama huna hela unaweza kuyachuja hata na kitambaa safi maalumu kwa ajili hiyo.
Ukiyachemsha maji unakuwa unaua viinilishe vingi mhimu vilivyomo ndani yake ambavyo mwili unavihitaji.
Mimi sijawahi kunywa maji ya kuchemshwa na sijawahi kuumwa tumbo wala sikumbuki mara ya mwisho niliumwa lini tumbo.
Chakula cha asubuhi cha mgonjwa wa vidonda vya tumbo:
Chagua kimojawapo kati ya hivi 7 nilivyoeleza katika mlo wako wa asubuhi
1. CHAI YA VIUNGO MBALIMBALI (SPICED TEA)
Chai ya mgonjwa wa vidonda vya tumbo inapikwa na kuandaliwa tofauti na ile ya mtu wa kawaida.
Jana nilifanya mahojiano na baadhi ya wagonjwa wa vidonda vya tumbo kupitia WhatsApp na niliwataka kila mmoja anieleze amekula nini au amepanga kula nini asubuhi.
Wachache walinipa majibu mazuri wengi wao wamenijibu vitu ambavyo sikutegemea kabisa yaani sikutegemea kama mgonjwa wa vidonda vya tumbo anaweza kunywa chai ya rangi na yenye sukari kwa amani zote kila siku bila wasiwasi wowote.
Mgonjwa wa vidonda vya tumbo anatakiwa aepuke vitu vyenye kaffeina na asidi nyingi.
Kwahiyo hutakiwi kutumia majani ya chai, hutakiwi kutumia kahawa au cocoa, hutakiwi kutumia sukari na hutakiwi kutumia vitafunwa vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi kama vile maandazi.
Chai yako andaa kwa vitu hivi > maji, tangawizi, mdalasini, iliki, mchaichai, na karafuu.
Hivi vyote vinaweza kuwa vya unga au siyo vya unga lakini bado vinaweza kuchanganywa pamoja na kukupa chai nzuri, chai ambayo ni dawa na isiyoweza kukuongezea vidonda vya tumbo.
Kama unapata vyote kwa pamoja yaani tangawizi, mdalasini, iliki, mchaichai na karafuu ni vizuri lakini hata ukitumia kimojawapo au viwili kati ya hivi kwa pamoja bado ni vizuri.
Unaweza pia kuongeza maji ya limau au ndimu au maji ya chungwa kijiko kidogo kimoja ndani ya chai hii.
Ulifundishwa ndimu au limau ni asidi?
Ndiyo, mwalimu wako alikuwa sahihi ila aliiangalia ndimu au limau likiwa mkononi au kwenye chombo ila ndimu na hata limau ukinywa maji yake yanapofika tumboni hubadilika na kuwa alkalini tena alikalini nzuri inayohitajika na mwili kuliko hata ile ya kwenye mboga za majani.
Ndimu au limau au machungwa ni matunda yenye vitamini C.
Vitamini C ni mhimu ili kuongeza kinga yako ya mwili na kinga yako ya mwili inapoongezeka uwezo wako wa kupona magonjwa mengi mwilini ikiwemo vidonda huongezeka sana, vitamini C pia huondoa sumu mwilini, hutibu majeraha na vidonda.
Ndiyo mgonjwa wa vidonda vya tumbo anaruhusiwa kutumia ndimu au limau.
Tangawizi ni dawa karibu kwa matatizo yote ya ndani ya tumbo.
Tangawizi imekuwa ikitumika na watu wengi kutibu matatizo mbalimbali ya tumbo kama vile kufunga choo au kupata choo kigumu, kuvimba tumbo, na kuondoa gesi tumboni.
Utafiti mmoja wa mwaka 2013 ulihitimisha kuwa tangawizi inaweza kutumika kupunguza maumivu ya vidonda vya tumbo vilivyotokana na bakteria wa vidonda vya tumbo ajulikanaye kama ‘H.Pylori bacteria’.
Kutumia au kuichanganya tangawizi kwenye vyakula unavyopika na kula mara kwa mara kunaweza pia kukusaidia kudhibiti vidonda vya tumbo vinavyotokana na asidi kuzidi mwilini.
Tangawizi husaidia kutibu dalili zinazojitokeza mwilini kama matokeo ya vidonda vya tumbo.
Tangawizi inamaliza na kuzuia kutokea kwa madhara anayoweza kuyapata mtu kama matokeo ya vidonda vya tumbo.
Kama unaumwa vidonda vya tumbo ukitumia tangawizi yenyewe kama ilivyo inaweza kukuletea maumivu zaidi hasa siku za kwanza unapoanza kutumia.
Ninakushauri usitumie tangawizi peke yake kama una vidonda vya tumbo.
Itumie kwenye chai kama hii yenye viungo vingine vingi ndani yake ili kuipunguza ukali wake.
Unaweza pia kutumia tangawizi na juisi ya matunda hasa juisi ya parachichi na uongeze asali ndani yake na siyo sukari na unaweza kunywa juisi hiyo kikombe kimoja kutwa mara 2 baada ya chakula.
Ndiyo mgonjwa wa vidonda vya tumbo anaruhusiwa kutumia tangawizi
Mhimu hapa ni marufuku kutumia sukari kama unaumwa vidonda vya tumbo.
Wewe mgonjwa wa vidonda vya tumbo tumia asali badala ya sukari.
Asali mbichi, ile nzuri kabisa ambayo haijachakachuliwa inao uwezo mkubwa katika kutibu vidonda vya tumbo.
Kama ujuavyo asali ni dawa karibu kwa kila ugonjwa.
Kuna kimeng’enya kilichomo kwenye asali kijulikanacho kama ‘glucose oxidase’ ambacho huizalisha ‘hydrogen peroxide’ ambayo yenyewe inayo uwezo wa kuuwa bakteria wabaya mwilini ambao husababisha vidonda vya tumbo.
Pia hii ‘glucose oxidase’ iliyomo kwenye asali huulainisha ukuta wa tumbo na kupunguza muwako au vidonda tumboni.
Asali ni dawa kabisa ya vidonda vya tumbo na nimesisitiza tangu mwanzo unatakiwa kula vyakula ambavyo tayari ni dawa.
Asali usiweke wakati chai ikiwa jikoni.
Asali iwekwe chai ikiwa kwenye kikombe na iwe imepoa kidogo kwani kwenye kimiminika cha moto sana asali hupungua uwezo wake wa kuwa dawa.
Asali pia unaweza kutumia kama mbadala wa bluebend au margaline.
Unaipakaa tu moja kwa moja kwenye silesi yako ya mkate.
Au changanya asali na mdalasini na utumie kama bluebend yako, unachukua asali lita moja na mdalasini ya unga vijiko vikubwa 8 changanya vizuri kabla ya kuitumia kila siku.
Kitafunwa kizuri kwako ni mayai ya kienyeji, mkate wa ngano ambayo haijakobolewa (brown bread) na chapati za unga wa ngano ambayo haijakobolewa na ukiweza hizi chapati zikandwe na tui la nazi na siyo maji matupu.
Vitafunwa vingine ni pamoja na ndizi za kuchemsha, ndizi nyama, ndizi nyama na nazi (tui), viazi vitamu vya kuchemsha, viazi vitamu vya nyama, viazi vitamu nyama na nazi (tui) au wali nazi.
Kumbuka nilisema siku za huko nyuma kuwa nazi ni chakula mhimu SANA kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo.
Mhimu pia mgonjwa wa vidonda vya tumbo asinywe maziwa iwe maziwa freshi au kwenye chai.
Chakula chetu cha asubuhi wagonjwa wa vidonda vya tumbo leo ni chai iliyopikwa kwa kutumia maji, mdalasini, mchaichai, iliki, tangawizi na karafuu.
Chai imeungwa kwa kutumia asali na kitafunwa tutachagua kati ya mayai ya kukaangwa (bila shaka utaongeza mboga mboga humo kama karoti, kitunguu maji, hoho nk) au mkate wa ngano ambayo haijakobolewa au chapati zilizokandwa kwa kutumia tui la nazi au ndizi za kuchemsha, ndizi nyama, ndizi nyama na nazi (tui), viazi vitamu vya kuchemsha, viazi vitamu vya nyama, viazi vitamu nyama na nazi (tui) au wali nazi.
2. UJI WA UNGA WA NDIZI
Kwenye ndizi ambazo hazijaiva (unripe bananas) kuna kitu kinaitwa ‘Sitoindosides’ na nimeshindwa kupata tafsiri yake kwa Kiswahili ni kitu ambacho hutengeneza ute kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na kuta za tumbo.
Ute ute huu hutoa ulinzi mkubwa kwa kuta za tumbo na kusaidia kuponya vidonda vya tumbo.
Ndizi ambazo hazijaiva pia huhamasisha kukua na kuzalishwa kwa seli kwenye utumbo mdogo.
Ndizi zina kiinilishe ambacho humeng’enywa na maji kijulikanacho kwa kitaalamu kama ‘Polysaccharides’, hii polysaccharides ni kiinilishe sawa na kile kinachopatikana kwenye dawa ya vidonda vya tumbo ya hospitali (ya kizungu) inayotolewa kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo iitwayo ‘Carafate’.
Ili kutibu na kudhibiti vidonda vya tumbo ukila ndizi ambazo hazijaiva unaweza kupata matokeo mazuri zaidi lakini matokeo mazuri zaidi yanapatikana ukitumia unga wake na utengeneze uji asubuhi.
Ili kupata unga wa ndizi menya ndizi kadhaa ambazo hazijaiva na ukate silesi ndogo ndogo kisha zianike juani kwa siku kadhaa mpaka zikauke kisha twanga kwenye kinu au saga hata mashineni upate unga mlaini zaidi.
Unaweza pia kukatakata silesi ndogo ndogo bila kuondoa ganda la nje la ndizi, yote ni sawa.
Unaweza kutumia unga huu kutengeneza uji wako wa asubuhi. Kumbuka unapopika uji huu usiive sana jikoni na usiungulie hata kidogo.
Kikombe kidogo kimoja (cha ujazo wa robo lita) kwa siku inatosha.
Kumbuka kuongeza asali kwenye uji huu na siyo sukari.
Kitafunwa kizuri kwako ni mayai ya kienyeji, mkate wa ngano ambayo haijakobolewa (brown bread) na chapati za unga wa ngano ambayo haijakobolewa na ukiweza hizi chapati zikandwe na tui la nazi na siyo maji matupu.
Vitafunwa vingine ni pamoja na ndizi za kuchemsha, ndizi nyama, ndizi nyama na nazi (tui), viazi vitamu vya kuchemsha, viazi vitamu vya nyama, viazi vitamu nyama na nazi (tui) au wali nazi.
3. SUPU YA KAROTI
Nimesema mara nyingi mgonjwa wa vidonda vya tumbo anahitaji zaidi ya asilimia 80 ya chakula chake kwa siku iwe ni mboga za majani na matunda
Kwa sababu hiyo nakuletea supu hii ya karoti kama mbadala wa supu ya nyama na kama tiba kwako mgonjwa wa vidonda vya tumbo.
Mahaitaji :
1. Karoti kubwa mbili au tatu
2. Kitunguu maji kikubwa kimoja na
3. Tui la nazi kikombe kimoja cha ujazo wa robo lita (ili kupata tui jingi na zito, ukishakuna nazi yako weka kwenye blenda na uongeze maji kidogo kisha blendi kwa dakika 10 hivi kisha chuja).
Nazi ni nzuri sana katika kutibu vidonda vya tumbo sababu ya sifa yake na uwezo wa kuua bakteria.
Nazi huwaua bakteria wanaosababisha vidonda vya tumbo na bakteria wengine wabaya mwilini.
Pia tui la nazi na maji ya nazi (dafu) vyote vina sifa na uwezo wa kutibu vidonda vya tumbo.
Namna inavyopikwa hii supu;
1. Zisafishe karoti zako na maji safi
2. Ondoa sehemu ya chini na juu kidogo,
3. Zikatekate vipande vidogo vidogo.
4. Menya kitunguu maji na ukatekate vipande vidogo vidogo.
5. Chukua sufuria weka maji nusu lita na tumbukiza ndani yake karoti, kitunguu maji na chumvi kidogo.
6. Weka jikoni na upike kwa dakika 10.
7. Ongeza tui lako la nazi ndani ya sufuria na uache jikoni kwa dakika 5 zaidi.
8. Ipua na uweke pembeni ipowe (unaweza kutumbukiza sufuria kwenye chombo kikubwa cha maji ili ipowe haraka.
9. Kisha mimina huo mchanganyiko wote kwenye blenda na usage kama unavyosaga juisi ya matunda, isiwe nzito sana wala isiwe nyepesi sana, ikiwa nzito ongeza kidogo tui la nazi.
10. Baada ya hapo mimina kwenye bakuli yako na supu na unywe ufurahie supu yako.
Kitafunwa kizuri kwako ni mayai ya kienyeji, mkate wa ngano ambayo haijakobolewa (brown bread) na chapati za unga wa ngano ambayo haijakobolewa na ukiweza hizi chapati zikandwe na tui la nazi na siyo maji matupu.
Vitafunwa vingine ni pamoja na ndizi za kuchemsha, ndizi nyama, ndizi nyama na nazi (tui), viazi vitamu vya kuchemsha, viazi vitamu vya nyama, viazi vitamu nyama na nazi (tui) au wali nazi.
Kumbuka nilisema siku za huko nyuma kuwa nazi ni chakula mhimu SANA kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo.
4. CHAI YA MCHAICHAI
Faida za mchaichai mwilini ni nyingi sana bali kwenye makala hii nitazieleza baadhi tu ambazo zina msaada wa moja kwa moja kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo.
Faida kubwa za mchaichai kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo ni pamoja na kuongeza kinga ya mwili, kutoa sumu mwilini, kutoa gesi mwilini, kuondoa tatizo la kukosa usingizi, kutibu matatizo mengi ya tumbo ikiwemo vidonda vya tumbo, homa, kudhibiti kisukari hasa kisukari aina ya pili, kudhibiti kolesto na kuondoa maumivu mbalimbali mwilini.
Mchaichai pia husaidia kuondoa uchovu sugu mwilini, kukupunguzia hamaki na hali za kupaniki vitu vidogo na kuondoa harufu mbaya ya kinywa na mwili kwa ujumla.
Mchaichai unadhibiti bakteria (anti-bacterial) unadhibiti pia fangasi (anti-fungal).
Ni mmea unatumika sana kusini mwa Asia, Afrika na Amerika.
Tafiti zinasema mchaichai unao uwezo wa kudhibiti bakteria mbalimbali wabaya wanaoleta maambukizi mwilini akiwemo bakteria anayesababisha vidonda vya tumbo ‘Helicobacter pylori’ na bakteria mwingine mbaya anayeleta magonjwa kama ya kuhara na maambukizi kwenye via vya uzazi vya mwanamke (PID) bakteria ajulikanaye kama ‘Escherichia coli’.
Mchaichai ni dawa nzuri sana ya asili kwa matatizo mengi ya tumbo ikiwemo kuondoa vivimbe tumboni, kutibu matatizo katika mmeng’enyo wa chakula, vidonda vya tumbo, kufunga choo au kupata choo kigumu, kuharisha, kujisikia uvivu na maumivu mengine ya tumbo.
Kwa mjibu wa utafiti mmoja wa mwaka 2003 mchaichai unao uwezo wa kusafisha mwili na kuondoa sumu mbalimbali kwakuwa hufanya kazi kama kikojoshi cha asili (natural diuretic properties).
Sumu zinapoondoka mwilini hurahisisha ogani mbalimbali za mwili kufanya kazi katika kiwango na uwezo wake wa juu kabisa ikiwemo kuongeza nguvu na afya ya figo na ini jambo linalosaidia pia kupunguza au kudhibiti ‘uric acid’ mwilini.
Ni dawa nzuri pia kwa maumivu mbalimbali ya mishipa.
Sote tunajuwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo na maumivu ni vitu usivyoweza kuvitenganisha.
Anaweza kupatwa na maumivu karibu kila sehemu ya mwili kama matokeo ya asidi kuzidi mwilini sababu ya vidonda vya tumbo.
Mchaichai unaondoa hayo maumivu bila shida yoyote.
Ni mmea unaoota kirahisi mazingira yoyote na huhitaji shamba ili kuwa nao.
Hapo hapo nyumbani kwako unaweza kupanda mchaichai kwenye kijinafasi kidogo tu na ukaendelea kufurahia chai yako ya mchaichai ambayo ni dawa na inakuletea harufu nzuri kwenye kinywa na mwili kwa ujumla.
Chai ya mchaichai inaandaliwa kwa kutumia maji, mchaichai wenyewe iwe ni mbichi au freshi kutoka kwenye mmea moja kwa moja au kama utapata mchaichai uliokaushwa na kuwa unga ni sawa na asali kama mbadala wako wa sukari.
Weka maji kwenye sufuria, tumbukiza mchaichai na weka jikoni mpake ichemke kisha ipua, chuja na subiri ipowe kidogo kisha ongeza asali ili kupata radha na furahia chai yako ambayo pia ni dawa.
Kitafunwa kizuri kwako ni mayai ya kienyeji, mkate wa ngano ambayo haijakobolewa (brown bread) na chapati za unga wa ngano ambayo haijakobolewa na ukiweza hizi chapati zikandwe na tui la nazi na siyo maji matupu.
Vitafunwa vingine ni pamoja na ndizi za kuchemsha, ndizi nyama, ndizi nyama na nazi (tui), viazi vitamu vya kuchemsha, viazi vitamu vya nyama, viazi vitamu nyama na nazi (tui) au wali nazi.
Asubuhi njema
5. SAHANI YA MATUNDA
Ndizi, tufaa na peazi
Kanuni ya jumla ya chakula cha mgonjwa wa vidonda vya tumbo kwa siku ni kuwa asilimia 80 ya chakula unachokula katika siku iwe ni mboga za majani na matunda.
Hii ni kusema kama jumla ya chakula unachokula kwa siku kina ujazo wa kilo 3 basi kilo 2 na nusu ziwe ni matunda na mboga za majani na nusu kilo iliyobaki ndiyo viwe vyakula vingine.
Watu wengi tunaposema kula matunda huwa wanawaza matunda mawili au tunda moja baada ya chakula.
Yaani tunda linakuwa kama kishushio tu au kitu cha ziada baada ya chakula.
Sasa kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo ni tofauti kwani mgonjwa wa vidonda vya tumbo matunda ndiyo inabidi yawe chakula kikuu kwake na vingine view ndiyo view vya ziada.
Yaani unaweza kuanza kula matunda mbalimbali mpaka ushibe halafu nyama au samaki au wali au ugali ndiyo kiwe kishushio au kitu cha ziada.
Kwa sababu hiyo nakushauri kama mgonjwa wa vidonda vya tumbo utenge kabisa mlo wako mmoja katika milo mitatu ya siku mlo huo uwe ni matunda tu bila kingine chochote na hii inawezekana kwa asubuhi au kwa usiku wakati mchana kula chakula cha kawaida cha kutosha.
Huku Tanzania hatuna utamaduni wa kula matunda asubuhi.
Huku asubuhi chakula kinachofikiriwa na kutumiwa na wengi kwa asubuhi ni chai kumbe kwa wenzetu wazungu asubuhi matunda ndiyo chakula kinachojulikana na wengi na chai ni kitu cha ziada.
Ukienda kwenye hotel nyingi za kitalii hapa Tanzania ni kawaida kuona sahani ya matunda (fruit plate) ni moja ya menu za vyakula vya asubuhi ambavyo mgeni anaweza kuagiza.
Seli ndani ya mwili lazima zibaki katika kiasi kidogo cha alkalini kutoka 7.2 mpaka 7.4, wakati 7.0 ni ya kati au husemwa sifuri katika kipimo cha PH (potential hydrogen). Chini ya 7.0 ni asidi na juu ya 7.0 ni alkalini.
Unaweza kukinunua kipimo cha PH na kupima Ph ya mate na mkojo, hii itakupa mwelekeo wa namna gani unafanya kuitunza 7.2 mpaka 7.4 kwenye seli ndani ya mwili wako.
Ikiwa mate yanasoma 6.0 au 6.5 ni kiashiria kuwa una asidi iliyozidi kwenye seli zako.
Moja ya sababu kuu ya mtu kutakiwa kula matunda ni kuwa vyakula hivi ni alkalini, wakati nyama, kuku, samaki, nyama ya nguruwe, pasta na mayai na vyakula vingine vingi ni asidi.
Miili yetu ilisanifiwa kula vyakula halisi vya asili (fresh natural grown food) au kula nyama iliyouliwa wakati huo huo (fresh live kill).
Masaa 24 kwa siku seli zinaunguza kaboni kama mafuta (cells burning carbon) ili kutuacha katika hali joto ya nyuzi joto 37.5.
Unapochoma kitu chochote, kinatoa nje taka moshi.
Taka zote hizo toka katika seli zote za mwili, lazima zirekebishwe kwa muda wa masaa yote 24 kwa msaada wa matunda.
Tumboni mwetu ndimo haidrokloriki asidi hutengenezwa na kuhifadhiwa ikisubiri kutumika wakati chakula kinaliwa.
Haidrokloriki asidi hii inahitajika na mwili ili kuuwezesha mwili kuyatumia madini yanayopatikana kwenye vyakula tunavyokula.
Baada ya hii haidrokloriki asidi kuwa imeandaliwa (opened up the food), valvu ya chini ya tumbo itajifungua na chakula huenda ndani mwanzoni mwa utumbo mdogo ambako asidi hupunguzwa makali (neutralized) na bikaboneti toka katika kongosho.
Ikiwa asidi hii haikurekebishwa vya kutosha na baadhi ya asidi inaingia katika utumbo mdogo, asidi hiyo itaziathiri seli na tishu na kwa kipindi cha muda mrefu itaathiri na kuziunguza kuta za tumbo na mwisho unapata vidonda vya tumbo vitokanavyo na asidi kuzidi mwilini.
Asilimia 90 ya watu wenye vidonda vya tumbo vimetokana na asidi na siyo bakteria.
Kwa sababu hiyo kuweka matunda kuwa sehehmu ya chakula chako kila siku ni ulinzi na uhakika wa kutosha katika juhudi zako za kutibu vidonda vya tumbo.
Kwa hiyo chakula chetu cha asubuhi leo jumamosi ni matunda tu mpaka tushibe na hakuna kingine zaidi.
Matunda ninayopendekeza zaidi kwako ni pamoja na peazi, tufaa (apple) parachichi, ndizi, machungwa na tikiti maji.
Matunda yanaondoa asidi mwilini, yanaondoa sumu kirahisi zaidi, yanaongeza kinga ya mwili, ni chanzo cha nyuzinyuzi (fiber) na husaidia pia kutibu majeraha ikiwemo vidonda vya tumbo.
Asubuhi njema
6. JUISI YA KABEJI
Vyakula vya asubuhi vya mgonjwa wa vidonda vya tumbo
Unahitaji kuwa makini na dawa na chakula unachokula kwa muda mrefu ili kupona vidonda vya tumbo.
Baadhi ya vyakula ambavyo nimekuwa nikivijadili hapa kama vyakula vya asubuhi kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo vinao uwezo wa kukuletea nafuu na kukutibu pia vidonda vya tumbo na moja ya vyakula hivyo ni Kabeji.
Sababu ya kuwa na viinilishe kadhaa maalumu, Kabeji inatajwa kama moja ya vyakula vinavyoweza kutibu vidonda vya tumbo.
Nitakueleza kwa kirefu namna kabeji inavyoweza kuwa msaada mkubwa kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo.
Juisi ya kabeji ni moja ya dawa mbadala au za asili ambayo imeandikwa sana kuwa na msaada mkubwa kwa watu wanaoumwa vidonda vya tumbo.
Kujiwekea utaratibu wa kunywa juisi hii kila mara ni namna nzuri ya kutibu na kudhibiti vidonda vya tumbo isiyo na gharama yoyote.
Juisi ya kabeji inatengenezwa kama unavyotengeneza juisi nyingine yoyote ya kawaida ya matunda.
Andaa juisi yako kwa hatua zifuatazo;
1. Toa ganda la juu la kabeji
2. Ioshe vizuri na maji yanayotiririka
3. Ikate vipande vidogo vidogo (chop) kisha tumbukiza kwenye blenda
4. Ongeza vipande vidogo vitatu au vitano vya karoti (ukipenda)
5. Ongeza maji kidogo ya kawaida
6. Saga juisi yako
7. Mwisho ichuje
8. Isiwe nzito sana wala nyepesi sana
9. Unaweza kuongeza kiasi kidogo cha maji ya limau au chungwa kupata radha
10. Juisi yako ipo tayari
Kwa matokeo mazuri zaidi ongeza asali na siyo sukari na ufurahie juisi yako na mlo wako wa asubuhi.
Kitafunwa kizuri kwako ni mayai ya kienyeji, mkate wa ngano ambayo haijakobolewa (brown bread) na chapati za unga wa ngano ambayo haijakobolewa na ukiweza hizi chapati zikandwe na tui la nazi na siyo maji matupu.
Vitafunwa vingine ni pamoja na ndizi za kuchemsha, ndizi nyama, ndizi nyama na nazi (tui), viazi vitamu vya kuchemsha, viazi vitamu vya nyama, viazi vitamu nyama na nazi (tui) au wali nazi.
Kwanini juisi ya Kabeji ni nzuri sana kwa mgonjwa wa vidonda vya tumbo?
• Kabeji ni chanzo kizuri cha lactic acid ambayo huongeza idadi ya bakteria wazuri kwenye mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula na kuwatupilia mbali bakteria wabaya wanaoweza kukuletea vidonda vya tumbo.
• Kabeji pia ina vitamini mhimu sana kwa kutibu vidonda na majeraha, Vitamini C ambayo pia hupunguza asidi mwilini.
• Hii hii kabeji ambayo wengine huiita sukuma wiki ina vitu vinne mhimu sana ambavyo hutibu, hulinda kuta za tumbo na mfumo wote wa mmeng’enyo wa chakula visishambuliwe na bakteria au asidi, vitu hivyo ni ‘L-glutamine’, ‘S-methylmethionine’, ‘glucosinolates’ na ‘gefarnate’.
• Kiasi cha kutosha cha ‘S-methylmethionine’ kilichomo kwenye kabeji husaidia pia kulitunza na kulipa ini afya bora.
• Hii glucosinolates iliyomo kwenye kabeji hutibu vidonda vya tumbo kwa kumuweka chini ya ulinzi bakteria anayeleta vidonda vya tumbo mwilini ajulikanaye kama ‘Helicobacter pyloribacteria’.
• Kitu kingine ambacho kabeji inacho ni ‘gefarnate’ ambayo yenyewe huulinda ukuta wa tumbo usipatwe na madhara jambo ambalo husaidia kutibu vidonda vya tumbo na matatizo mengine mengi yahusuyo tumbo.
• Kabeji inasaidia kuweka sawa usawa wa asidi na alkalini mwilini (pH balance). Imethibitika kuwa kitendo hiki husaidia pia kuondoa gesi tumboni.
• Kabeji pia inao uwezo wa kuzuia shida na misukosuko yoyote ya tumbo ikiwemo damu kuvuja tumboni kama matokeo ya vidonda vya tumbo (anti-inflammatory properties).
Juisi ya kabeji pia ni dawa nzuri ya saratani, kolesto na husaidia sana mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Mhimu pia mgonjwa wa vidonda vya tumbo asinywe maziwa iwe maziwa freshi au kwenye chai.
Asubuhi njema
Ikiwa makala hii inakusaidia kuboresha maisha na afya yako kwa namna moja au nyingine na unapenda kutoa shukrani au zawadi kwangu tuwasiliane kwenye WhatsApp +255714800175 nitakupa maelekezo namna ya kunitumia zawadi yako hiyo.
Umependezwa Na Makala Uliyoisoma? Niachie Maoni yako Hapa Chini.
Endelea Kufuatilia Makala Zingine Zinazotolewa na mimi kwenye Blog Hii.
Nashukuru sana kwa masomo yako
Karibu sana ndugu
Vyakula vyamucha ni nini
Safi sana 🙏tunajifunza mengi
Karibu sana ndugu
Je ni unga gani n sahihi kwa mtu mwenyewe vidonda vya tumbo … ni dona au sembe
Dona ndiyo mzuri zaidi