Last Updated on 17/11/2021 by Tabibu Fadhili Paulo
Jinsi ya kuimarisha afya ya mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula
Ili kuimarisha mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula unahitaji kula zaidi vyakula vyenye bakteria wazuri.
Tumboni kwako kuna bakteria wa aina mbili, bakteria wazuri na bakteria wabaya na kwa bahati mbaya mwili au tumbo lako linawahitaji bakteria wote wawili yaani bakteria wazuri na bakteria wabaya ili uendelee kuishi.
Hata hivyo kwa bahati mbaya watu wengi wanakuwa na bakteria wabaya wengi kuliko bakteria wazuri na hapo ndiyo huwa chanzo kikuu cha magonjwa mengi mwilini kama PID, vidonda vya tumbo, bawasiri, amiba, magonjwa ya virusi, kushuka kwa kinga ya mwili na mengine mengi.
Ili kuepuka yote hayo unahitaji kuwa unakula vyakula vyenye bakteria wazuri mara kwa mara ili kuweka usawa mzuri wa bakteria tumboni mwako.
Asilimia zaidi ya 70 ya kinga yako yote ya mwili ipo kwenye kuta za tumbo lako.
Hii ni kusema linapokuja suala la kuwa na kinga nzuri ya mwili na inayofanya kazi kukulinda unahitaji kuwa makini namna unavyotunza usawa huu wa hawa bakteria tumboni mwako.
Tumbo lako ndiyo injini ya mwili wako. Maisha yako yote yapo tumboni na kila chakula na kinywaji hufika kwanza tumboni kabla hakijameng’enywa na kusambazwa sehemu zingine za mwili.
Kwahiyo jambo lolote linaloharibu afya yako ya tumbo ujuwe linaharibu pia kinga yako ya mwili na kukuweka karibu na magonjwa mengine mabaya kama vidonda vya tumbo, bawasiri, saratani ya tumbo, kuishiwa kinga ya mwili na mengine mengi.
Jinsi ya kuimarisha afya ya mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula
Ili kuimarisha mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula unahitaji kula zaidi vyakula vyenye bakteria wazuri.
Vyakula vyenye bakteria wazuri vimegawanyika mara mbili.
Kuna vyakula vyenyewe vyenye hao bakteria wazuri ambavyo hujulikana kwa kiingereza kama ‘Probiotics’ na kuna vyakula ambavyo ni chakula cha hao bakteria wazuri ambavyo kwa kiingereza hujulikana kama ‘Prebiotics’.
Probiotics ni vyakula vyenye bakteria wazuri na Prebiotics ni chakula ambacho hao bakteria wazuri wanakula.
Probiotics ni jeshi, wakati Prebiotics ni chakula cha hao wanajeshi.
Probiotics ambao ni bakteria wazuri wanaulinda mji wako wa tumbo na kukuimarishia kinga yako ya mwili na ubongo.
Bakteria wazuri wanahusika pia kushusha msongo wa mawazo (depression) na kuimarisha afya ya moyo.
Bakteria hawa wazuri pia tafiti mbalimbali zinasema wanaweza pia kukufanya uonekane una ngozi nzuri na ya kuvutia.
Vipo vidonge vyenye hawa bakteria wazuri (supplements) lakini bado nakushauri uwapate kupitia chakula moja kwa moja.
VYAKULA VYENYE BAKTERIA WAZURI – PROBIOTICS
Kwa bahati mbaya kwa hapa kwetu Tanzania vyakula vyenye bakteria wazuri na vinavyopatikana kirahisi ni chakula kimoja tu nao ni MTINDI.
Mtindi pekee ndiyo chakula chenye bakteria wazuri kinachopatikana kirahisi hapa Tanzania.
Mtindi ni moja ya vyakula vizuri kabisa vyenye bakteria wazuri ambao wanaweza kuimarisha afya ya mmeng’enyo wako wa chakula.
Mtindi unatokana na maziwa ya ng’ombe.
Kula mtindi mara kwa mara kuna uhusiano wa kuimarisha afya yako ya mwili ikihusisha afya ya mifupa. Mtindi una faida nyingi pia kwa watu wenye shinikizo la juu la damu.
Kwa watoto wadogo mtindi unaweza kusaidia kupunguza tatizo la kuharisha lililotokana na matumizi ya dawa za antibiotics.
Mtindi pia unaweza kutumika kwa watu wenye aleji na maziwa fresh ya kawaida (lactose intolerance).
Mtindi mzuri kabisa ni ule uliotengeneza mwenyewe nyumbani.
Lakini unaweza kutumia pia mtindi wa dukani hasa mtindi wa Tanga Fresh nakuruhusu unaweza kutumia.
Kama utatumia mtindi wa dukani uwe ni wenyewe peke yake usiwe umeongezwa rangi wala sukari au kingine chochote.
Robo lita (ml 250) kwa siku ni kiasi sahihi cha mtindi kwa watu wengi.
Vyovyote itakavyokuwa usizidishe Zaidi ya mtindi nusu lita (ml 500) kwa siku.
Watu wenye vidonda vya tumbo wanaruhusiwa kula mtindi isipokuwa maziwa fresh ndiyo hawatakiwi kunywa.
VYAKULA VYA BAKTERIA WAZURI – PREBIOTICS
Hivi ni vyakula sasa kwa ajili ya hao bakteria wazuri na unavihitaji kwa wingi ili hao bakteria wazuri wawe na nguvu za kufanya kazi zao vizuri kama inavyowapasa.
Prebiotics vinatoka katika baadhi ya vyakula vya wanga hasa wanga wenye nyuzinyuzi (fiber) navyo ni pamoja na vyakula vifuatavyo;
• Mboga za majani
• Ndizi. Ndizi zenyewe kama zilivyo au ukipata unga wake unaweza kutengeneza uji wa unga wa ndizi
• Maharage
• Kitunguu swaumu
• Kitunguu maji
• Vyakula jamii ya kunde
Vitu vingine vinavyoimarisha afya ya mmeng’enyo wa chakula:
Pia unaweza kuimarisha afya ya mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula kwa kufanya yafuatayo (namba 6 ni mhimu zaidi)
- Kunywa maji glasi 2 (nusu lita) mara tu uamkapo kutoka kitandani kila siku. Kunywa tena kiasi hiki cha maji kila nusu saa kabla ya chakula cha asubuhi, mchana na cha jioni kila siku.
- Kula chakula kichache milo mingi. Kula hata mara 5 kwa siku lakini chakula kidogo kidogo siyo kingi kwa wakati mmoja.
- Kula pole pole ulapo chakula
- Hakikisha unapokula chakula huna mawazo mawazo (stress) yoyote.
- Kula zaidi vyakula vyenye nyuzi nyuzi
- Punguza kukaa chini au kwenye kiti masaa mengi
Mawasiliano yangu ni WhatsApp +255714800175
Mjulishe rafiki yako kwenye Twitter naye asome makala hii kwa kubonyeza maneno yafuatayo;
Jinsi ya kuimarisha afya ya mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula Share on XSHARE POST HII NA WENGINE UWAPENDAO